Nabi alisema, wiki kadhaa nyuma Morrison
alionekana kuwa hovyo licha ya kumwandalia programu maalumu ya kujiweka fiti,
lakini kwa sasa anavyomwona mazoezini na hata kwenye mechi za kirafiki
anaonekana ameiva tayari kuleta balaa uwanjani dhidi ya wapinzani wa Yanga.
Kocha huyo alisema baada ya kuona Morrison
hawa kiwango alichokitaka, alimpangia programu maalumu ya kufanya mazoezi ya nguvu
akiwa chini ya Kocha wa Viungo, Helmy Gueldich ambayo sasa imeonekana kuwa na
faida kwake.
“Alivyo Morrison wakati huu ni tofauti na
awali alipojiunga na kikosi, programu maalumu ya mazoezi imemsaidia na kuongeza
utimamu wa mwili wake katika kushindana ingawa hajafika pale ninapohitaji kumwona,”
alisema Nabi na kuongeza;
“Naamini Morrison akiwa fiti asilimia
kubwa, kwanza atacheza mechi mfululizo akiwa katika kiwango cha juu tofauti na
michezo mitatu ya kimashindano aliyocheza hadi sasa ndani ya kikosi chetu.”
“Miongoni mwa wachezaji waliofanya vizuri
katika kikosi chetu kwa sasa Morrison ni mmoja wapo amefunga bao moja na kutoa
pasi ya mwisho moja, amehusika kwenye mabao mawili muhimu yaliyochangia kutupa
pointi sita Ligi Kuu tena michezo migumu ya ugenini.
“Kama
akifika katika utimamu wa mwili na kuwa fiti kama ninavyohitaji kutoka kwake,
atakuwa kwenye kiwango bora zaidi ya misimu yote mitatu aliyocheza soka hapa
nchini.”
Nabi pia alisema Morrison ana uwezo wa
kutengeneza nafasi za kufunga na muda mwingine kufanga mabao aina mbalimbali na
uwepo wake uwanjani muda mwingi unawapa wakati mgumu wapinzani.
Nabi alisema ikitokea kuna nafasi nyingine
mashindano kusimama kama ilivyo kwenye wiki mbili hizi atakuwa anatengeneza
ratiba nyingine ya kumwandaa Morrison kama ilivyofanya katika wakati huu.
“Tunahitaji kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa na yale ya ndani uwezo wa wachezaji kama Morrison tena akiwa fiti itakuwa na faida kwetu kufikia malengo hayo tuliyojipangia,” alisema.
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Timu ya Wananchi App kwenye Simu Yako Upate Habari Za Timu yako Kwa Haraka Zaidi