Licha ya matumaini makubwa waliyokuwa nayo mashabiki na wapenzi wa Yanga Sc, mambo yalienda kombo baada ya timu hiyo kulazimishwa suluhu nyumbani ikiwa ni mwendelezo wa mzimu wa kutokuwa sawa katika michuano ya Afrika kila inapotia mguu.
Yanga Sc ikicheza nyumbani ililazimishwa suluhu na
Club Africain ya Tunisia katika mchezo wa kwanza wa hatua ya mtoano (play-off)
wa Kombe la Shirikisho Afrika.
Matokeo hayo yanakuja ikiwa timu hiyo
ikitoka kutupwa nje ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kufungwa na Al Hilal ya
Sudan kwa jumla ya mabao 2-1, ikilazimishwa sare ya 1-1 na kulala 1-0 ugenini
na kuangukia hatua hiyo ya play-off ya shirikisho ambapo imeanza kwa suluhu.
UCHOVU ULIONEKANA
Katika mechi ya juzi,
Yanga Sc haikuwa na mzuka kama ilivyokuwa dhidi ya Al Hilal ikiwa nyumbani,
kwani nyota wake walionekana kuwa wachovu pengine kutokana na fatiki ya kucheza
mechi mfululizo za Ligi Kuu Bara.
Yanga imecheza mechi
nne ndani ya muda wa siku 10, hii ni ratiba ngumu kuanzia Oktoba 23 ilipocheza
dhidi ya Simba kisha siku tatu baadaye ikacheza dhidi ya KMC, kabla ya kusafiri
tena hadi Mwanza kucheza na Geita Gold na kugeuza kuwahi mchezo huo wa juzi.
Hii ni ratiba ngumu
ambayo ni vigumu kwa klabu yoyote kucheza kwa ubora na kupata matokeo bora
katika mlundikano wa namna hiyo.
Yanga ilionekana
kuathirika na uchovu mapema tu baada ya wapinzani wao kucheza soka la kujihami
na kujilinda ambapo walikosa ubora wa kuufungua ukuta wao na kupata mabao kama
ambavyo walikuwa wanatamani.
Ukiangalia winga
Bernard Morrison, Stephane Aziz KI, Feisal Salum, Fiston Mayele walijieleza
wazi jinsi ya mchoko ulivyowaathiri katika mchezo huo wa juzi, hawakuwa na
utulivuy kichwani wa ubunifu wa kupenya ngome ya Club Africain.
TUISILIA BADO SANA
Winga Tuisila Kisinda
alistahili kutolewa mapema katika mchezo huo ni bahati kwake kumaliza dakika 45
za kwanza kutokana na kutokuwa na jipya. Mtaji wake mkubwa ulikuwa ni mbio na
hakukuwa na nafasi ya kufanikisha hilo kutokana na wapinzani wao hawakuwa na
akili ya kushambulia kabisa na mabeki wao wa pembeni kuvuka hata nusu ya
uwanja.
Kisinda hakuwa na
mbinu nyingine za kupenya na hata alipopata nafasi ya kutaka kukimbia mbio zake
alijikuta ameshaumaliza uwanja na kuonekana wa kawaida.